PASAKA YA MSAMAHA, MATUMAINI NA UPENDO: Sauti ya ARIMO kwa Wanataaluma, Wanafunzi na Wafanyakazi

Posted On: 18, April 2025

Wakati Watanzania – Wakristo na wasio Wakristo – wakiungana na watu wa mataifa mengine kusherehekea siku kuu ya Pasaka kama tukio la kipekee la mapumziko, tafakari na mabadiliko, Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) kama taasisi ya umma kinatoa ujumbe murua wa Pasaka unaosisitiza msamaha, matumaini na upendo. Kwa mwaka huu wa 2025, viongozi wa chuo, wanafunzi na wafanyakazi wameshikamana kusisitiza kwamba Pasaka ni zaidi ya siku kuu ya kiroho kwa waumini wa Kikristo; wanaiona kuwa fursa ya kujenga jamii shirikishi, yenye neema na tija.

Akiongea na safu hii, Mkuu wa Chuo - Bwana Charles Saguda - anaiomba jamii kutumia sherehe za siku kuu ya Pasaka kama njia ya kutuwezesha kufanya mahusiano yetu ya kazi kuwa mapya. “Kipindi cha Pasaka kitupe wasaa wa kusamehe makosa yaliyopita na kutoa nafasi ya kuanza upya. Tunapopokea msamaha, tunawaweka wenzetu huru na kujivunia utu wa pamoja.” Bwana Saguda anaelezea kuwa vyombo vilivyobebwa katika sinia vinaweza kugongana lakini havivunjiki. Msamaha utusaidie kutovunjika moyo kutokana na migongano ya hapa na pale, bali tuendelee kuwa wamoja kukijenga chuo na kuhudumia jamii.

Kwa upande mwingine, Profesa Ernest Kihanga, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri, anachora picha ya chuo kinachojali imani na maono ya pamoja, bila kujali asili au imani binafsi. Amenukuliwa akisema, “Mtu anaweza kutafsiri Pasaka kwa njia yake, lakini kama taasisi tafsiri yetu inajikita katika kushirikiana kwa lengo moja: kujenga ARIMO yenye nguvu, ubunifu na mshikamano.” Profesa Kihanga anawaasa wanataaluma kushirikiana katika kufanya machapisho na kutafuta miradi kwa mustakabali wa chuo.

Kama daraja linalounganisha uongozi wa chuo na wanafunzi, Rais wa Serikali ya Wanafunzi, Bwana F. Barabara, anaielezea siki kuu ya Pasaka kama darasa la ustawi na uwajibikaji. “Ni wakati wa kutambua kwamba elimu siyo tu masomo darasani, bali pia kujitolea kwa jamii”. Bwana Barabara anaeleza kuwa, “Pasaka inatukumbusha kuwa tumekuwepo ili kubadilisha maisha ya watu.”

Naye Bi. Happiness Magambo, Mshauri wa Wanafunzi, anaongeza: “Tunaweza kuchukua msamaha na matumaini ya Pasaka kuwa mwanzo wa kujifunza kwa upendo, ujasiri na uongozi unaokusudiwa kuleta mabadiliko chanya.” Bi. Magambo anatuasa kutumia kipindi cha Pasaka kutafakari namna bora ya kutekeleza mipango ya chuo huku tukizingatia haki na usawa.

Bwana Najum Juma, ni Mkuu wa Idara ya Taaluma. Anasisitiza umuhimu wa wanataaluma na wanafunzi kuzingatia weledi na maadili katika kazi zetu za kila siku. Akiungana na viongozi wakuu wa chuo, anaona umuhimu wa kusameheana pale tulipokwazana. “Kitaaluma, msamaha ni daraja la kujenga mashirikiano, na pia ni kiwanda cha mawazo chanya”. Bwana Najum anaamini kuwa jamii ya wanataaluma wanaopendana na kushirikiana wana nafasi ya kufanya utafiti na ubunifu unaoleta maendeleo kwa chuo na kwa jamii.

Safu hii ilipata bahati ya kuzungumza na Bi. Veronica ambaye ni Mtaalam wa Upangaji Miji. Yeye ni miongoni mwa wanataaluma wa Chuo cha Ardhi Morogoro mwenye ari kubwa ya kufundisha na kuendesha miradi. Yeye katika kuitafakari siku ya Pasaka anatuambia, “Tunapochukua nafasi ya kutafakari, tunaweza kukiona Chuo kama mwili mmoja. Kila sehemu ya mwili huwa ina jukumu lake, vivyo hivyo kila Idara na kitengo chuoni vina majukumu yake”. Bi Veronica anadai kuwa Pasaka inatufundisha kutengeneza mazingira yanayoinua maisha na ustawi wa kila mfanyakazi, mwanafunzi na kiongozi.

Chama cha wafanyakazi kupitia kiongozi wake, kilitoa salamu za heri kwa siku kuu ya Pasaka pia. Bwana Katemi Patrick, Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi (RAAWU), anasisitiza uwazi na haki kazini. “Wafanyakazi wenye haki na usalama wanajifunza kuaminiana na taasisi yao. Pasaka inapopiga doria, inatuambia tuweke vigezo vya haki, mshikamano na uwajibikaji.” Bwana Katemi anawaomba wafanyakazi kusaidiana na viongozi wa RAAWU katika kujenga jamii inayojali haki na ustawi wa kila mmoja.

Katika kila kauli, Pasaka inaonekana kama mwangaza unaotufahamisha kuwa Msamaha na Upendo huanzisha mchakato wa kuondoa tofauti zetu na kujenga daraja kati ya wote – wafanyakazi na viongozi, wanataaluma na wanafunzi. Pasaka imebeba wito wa kutuasa kuachana na uzembe, fitina, na ufisadi na kulenga kwa pamoja kufikia malengo ya chuo.

Hivyo basi, Pasaka si tukio moja tu bali msukumo wa maisha mapya, kama mvua inayoleta maji ardhini, ikiwezesha mimea mipya kumea. Kwa maneno yao, viongozi, wanafunzi na wafanyakazi wa ARIMO wanawaalika wote – wakristo na wasio Wakristo, wasomi na wafanyabiashara – kusherehekea Pasaka 2025 kwa pamoja, huku tukisameheana na kupendana.

ARIMO inawatakia wote Pasaka yenye furaha, utulivu na ari ya kujenga jamii bora.